Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu

(DSFA)

Tanzania yang'ara mipango ya Uchumi wa Buluu Kimataifa

Imewekwa: 25 July, 2025
Tanzania yang'ara mipango ya Uchumi wa Buluu Kimataifa

Katika mkutano wa pembezoni  (side event) wakati wa kikao cha thelathini  cha nchi wanachama wa  Mamlaka ya Kusimamia Sakafu ya Bahari Kuu ya Kimataifa (International Seabed Authority - ISA) kilichofanyika Kingston, Jamaica kuanzia tarehe 21-25 Julai, 2025; Tanzania iliwasilisha ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia kwa nchi katika kunufaika na fursa za Uchumi wa Buluu.
Tukio hilo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), ISA na Benki ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Teknolojia kwa Nchi zinazoendelea (UNTB- LDC) tarehe 24 Julai, 2025 katika Makao Makuu ya ISA, Kingston - Jamaica.
Akihutubia  wakati wa tukio hilo, Kapt. Hamad Bakar Hamad, Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi (Zanzibar ) alieleza namna Serikali zote mbili zilivyojipanga  kuwa na sera nzuri zinazomwezesha mwananchi kunufaika na fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu. Vilevile alieleza kuwa matokeo na mapendekezo ya ripoti hii yatachochea hatua mbalimbali ambazo Serikali imeshaanza kuchukua katika kuhakikisha kwamba Uchumi wa Buluu unaongeza mchango wake kwenye pato la Taifa. Mwisho, alihitimisha kwa kuishukuru UNTBLDC na ISA kwa mchango wao katika kutekeleza mradi tajwa na aliwakaribisha wadau wa maendeleo kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo. 
Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman, Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, NewYork alisisitiza msimamo wa Tanzania kuendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na mashirika yake katika mipango mbalimbali ya maendeleo hususani utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hususani SDG14: "Uhai Chini ya Maji" kwa maana ya Kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu bahari na rasilimali za baharini kwa maendeleo endelevu.
Awali, akihutubia wakati wa ufunguzi wa tukio hilo Bi. Leticia Carvalho, Katibu Mkuu wa ISA aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo muhimu. Ripoti hiyo itakuwa rejea (benchmark) kwa ISA na UNTBLDC katika kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea kuwa na mipango mahususi ya kunufaika na fursa zitokanazo na Uchumi wa Buluu. Kwa namna ya pekee, aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa na Wizara mahususi ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi. Akihitimisha  hotuba yake, alitoa ahadi ya kuwaunganisha wadau wa maendeleo na Serikali  ya Tanzania ili kutekeleza mapendekezo yaliyopo katika ripoti na kuahidi ushirikiano wa ISA hatua kwa hatua.
Wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya ripoti hiyo, Dkt. Emmanuel Sweke alieleza kuwa mchakato ulihusisha Wataalam kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na asasi za kiraia, ambapo UNTBLDC na ISA walitoa mkandarasi mshauri. Mradi huo wa uandaaji wa ripoti ya tathmini ya mahitaji ya teknolojia ulichukua muda wa miaka miwili na ulikuja na mapendekezo ya sekta mbili, Uchumi wa Buluu na Kilimo na sekta mtambuka za Madini na uchakataji. Vilevile, alieleza kuwa tayari mapendekezo ya miradi minne ambayo ni Ufuatiliaji wa Kielekteoniki wa meli za Uvuvi, mnyororo wa thamani wa baridi, kanzi data ya takwimu na kujengewa uwezo.
Utekelezaji wa ripoti hii utakuwa moja ya kichocheo cha mapinduzi ya fursa za Uchumi wa Buluu na Kilimo nchini Tanzania.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo