Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu

(DSFA)

Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani

Imewekwa: 21 November, 2025
Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, alisema kuwa uuzaji wa samaki nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 42,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 509.9 hadi tani 59,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 755. Sambamba na hilo, idadi ya wavuvi imeongezeka kutoka 198,475 mwaka 2023 hadi 201,661 mwaka 2024. Idadi ya viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nayo imeongezeka kutoka 21 hadi 64 katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024. Hayo aliyasema leo Novemba 21, 2025, alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani jijini Dar es Salaam katika fukwe za Kawe Beach kwa lengo la kuhamasisha dhana ya Uchumi wa Buluu, ulaji wa samaki na mazao yake, pamoja na kuimarisha shughuli za uhifadhi wa mazingira na rasilimali za uvuvi yaliyofanyika kwa muda wa siku 2 kuanzia tarehe 20 hadi 21 Novemba 2025.

Katibu Mkuu aliendelea kusema kwamba, Serikali itaendelea kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, ufugaji wa samaki kwa njia za vizimba na mabwawa, pamoja na kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa samaki, kupunguza uharibifu wa mazingira, kuzuia uvamizi wa fukwe na kupunguza shinikizo la uvuvi.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu amezindua mpango wa kitaifa wa usimamizi wa samaki aina ya Jodari na mpango wa uhifadhi wa samaki aina ya papa na taa, pamoja na kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho kujionea bidhaa za mazao ya uvuvi.

Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo “Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Endelevu: Msingi Imara wa Uchumi wa Buluu.”

Mrejesho, Malalamiko au Wazo