Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu

(DSFA)

Mkutano wa 15 wa Kamati ya Kitaalam ya Vigezo vya Ugawaji (TCAC15) ya Tume ya Tuna ya Bahari ya Hindi (IOTC)

Imewekwa: 18 July, 2025
Mkutano wa 15 wa Kamati ya Kitaalam ya Vigezo vya Ugawaji (TCAC15) ya Tume ya Tuna ya Bahari ya Hindi (IOTC)

SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema licha ya nchi kuwa na eneo kubwa la bahari kuu na utajiri mkubwa wa rasilimali ya samaki aina ya jodari, bado haijafaidika ipasavyo kiuchumi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi SMT, Agnes Kisaka Meena, ameyasema hayo wakati akifungua mkutano 15 wa kimataifa wa kamati ya ufundi kuhusu vigezo vya mgao wa rasilimali ya kamisheni ya Uvuvi wa Samaki wa Jodari katika Bahari ya Hindi uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip. Alisema soko la samaki hao kimataifa lipo na ndio maana Tanzania imeamua kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa lengo la kuona wanafikiwa na kuongeza kiwango cha uvunaji ili kusaidia kuongeza uchumi wa nchi.

Alisema Tanzania ina sera ya uchumi wa buluu ambayo inahimiza kuhakikisha mazao ya baharini yanatumia kusaidia ongezeko la uchumi. “Tuna eneo kubwa la bahari na lina samaki wengi wa jodari, lakini hatujafanikiwa kuwanufaisha Watanzania kiuchumi kwa kiwango tunachotegemea”, alisema. Agnes alifahamisha kuwa kuwa lengo la mkutano huo ni kufanya majadiliano ya pamoja kwa kuzingatia tafiti za kisayansi, takwimu na kutoa ushauri kwa kamisheni. Aliahidi kuwa serikali imedhamiria kushirikiana na wadau wa kimataifa na kikanda ili kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika zaidi na uvuvi wa bahari kuu, hususan kupitia matumizi ya teknolojia katika uvuvi na usindikaji wa mazao ya baharini.

Naye Katibu Mtendaji Tume ya Samaki wa Jodari Bahari ya Hindi, Paul De Bruyn, alisema anaimani mkutano huo utaleta matokeo mazuri, kwani kwa takriban miaka 10 wanafanya vikao kujadili namna ya kuwa na uvuvi endelevu utakaoleta tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emanuel Andrew Sweke, alisema kati ya wanachama 30, Tanzania imekuwa mstari wa mbele wakiongozwa na kauli mbiu na utashi mkubwa wa viongozi kuhakikisha rasilimali waliyojaaliwa na Mwenyezimungu waweze kufaidika nayo. Jambo jengine alisema serikali zimeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta hiyo na matakwa ya kujenga bandari za uvuvi Tanzania bara na Zanzibar.

Alisema matumaini yake ni kwamba mkutano huo utaleta mafanikio makubwa kwa nchi na wananchi wa Tanzania kuweka uendelevu wa samaki hao kutosheleza kwa ajili ya mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Zahor Kassim Alharusi, alisema Tanzania ni moja ya nchi iliyopo kwenye jumuiya hiyo na ina rasilimali kubwa ya bahari ambayo ina samaki aina ya jodari.

Alisema ili kuwahifadhi na kuhakikisha wanaendelea kuvunwa ni lazima kuwa na mashirikiano ya nchi zote zinazojishughulisha na uvuvi wa samaki hao.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo